Uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kumuongezea muda Prof. Ibrahim Hamis Juma kuendelea kuwa Jaji Mkuu Nchini hauvunji Katiba kama ilivyofanyiwa marekebisho.
Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu, uliotolewa 22 Septemba 22, 2023, wa Jaji Godfrey Isaya kutupilia mbali kesi ya kikatiba iliowasilishwa na mleta maombi, ambaye ni Mwananchi wa kawaida Humphrey Malenga.
Alisema, “Rais ana mamlaka kwa mujibu wa Ibara ya 120 (3) inayosomwa pamoja na Ibara ya 118 (2) ya Katiba ya kuongeza muda wa Jaji wa Rufani ili kumwezesha kuendelea kutekeleza majukumu yake. Naona maombi hayana mashiko. Nayatupiliwa mbali.”
Mleta maombi huyo, alitaka amri ya kutafsiri masharti ya Ibara ya 118 (2) ya Katiba kuhusu umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu kuwa miaka 65 na si umri wa kustaafu kwa Jaji wa Rufani na pia kutaka tafsiri ya kifungu hicho kuwa ni Ibara inayosimama pekee na haihusanishwi na masharti ya Ibara ya 120 (1) (2) (3) na (4) ya Katiba wakati wa kuamua muda au umri wa kustaafu kwa Jaji Mkuu.
Aidha, mwombaji aliomba tafsiri ya mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kusimamisha umri wa kustaafu wa Jaji wa Mahakama ya Rufani au kuongeza muda wa utumishi wa Jaji wa Rufani kwa maslahi ya umma kwa mujibu wa Ibara ya 120 (2) na (3) haimhusu Jaji wa Rufani ambaye pia ni Jaji Mkuu.
Katika hukumu yake, Jaji Isaya alisema kuwa Ibara ya 118 ya Katiba haiwezi kusomwa peke yake, bali inasomwa pamoja na Ibara ya 120 ya Katiba, hivyo mamlaka ya Rais kuongeza muda wa Jaji Mkuu wa sasa madarakani yalikuwa sahihi, hivyo yako sambamba na Katiba.