Mashetani wekundu (Manchester United) wanatajwa kujianda na vita ya usajili wa wachezaji kutoka nchini Croatia, ambao walifanikisha safari ya taifa hilo kufika hatua ya fainali katika michuano ya kombe la dunia huko Urusi Ivan Perisic na Ante Rebic.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na gazeti la The Sun la England, meneja Jose Mourinho ameanza kuuchochea uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha wawili hao wanatua Old Trafford, kabla ya dirisha kufungwa kwa dirisha la usajili mapema mwezi ujao.
Mourinho amewahi kuhitaji huduma ya Perisic msimu uliopita, lakini alikumbana na vikwazo kutoka kwa viongozi wa klabu ya Inter Milan, lakini kipindi hiki amedhamira kuung’oa mzizi wa fitna.
Kwa upande wa mshambuliaji Rebic mwenye umri wa miaka 29, itakua changamoto mpya kwake, endapo uongozi wa Man utd utawasilisha ofa kwenye klabu ya Eintracht Frankfurt inayotumikiwa na mchezaji huyo.
Tathmini ya awali iliyoandikwa kwenye taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti la The Sun imeonyesha kuwa, thamani ya wachezji hao wawili kwa pamoja huenda ikaigharimu Man utd kiasi cha Pauni milioni 92.
Rebic na Perisic jana jumatatu, walikua kivuti kwa mashabiki wa soka nchini Croatia wanaoakadiriwa kufikia 100,000 walijitokeza wakati wa mapokezi ya timu mjini Zagreb.
Perisic alifunga bao la kwanza katika mchezo wa fainali kabla ya mshambuliaji Mario Mandzukic hajafunga bao la pili la kufutia machozi dhidi ya Ufaransa, ambao walichomoza na ushindi wa mabao manne.
Taifa la Croatia limefanikiwa kucheza fainali ya kwanza ya kombe la dunia katika historia ya soka duniani, baada ya kuishia kwenye nafasi ya tatu wakati wa fainali za kombe la dunia mwaka 1998.