Klabu ya Manchester United imemsajili mshambuliaji wa zamani wa klabu ya Watford Odion Ighalo, akitokea Shanghai Shenhua inayoshiriki ligi kuu ya Chana kwa mkopo wa miezi sita.
Klabu ya Manchester United imekamilisha dili la mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, huku ikipewa nafasi ya kumsajili moja kwa moja endapo itaridhishwa na kiwango chake, hadi mwishoni mwa msimu huu.
Mpaka jana Ighalo, bado alikua nchini China, lakini alitarajiwa kuanza safari ya kuelekea England, kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kujiunga na mashetani wenduku wa Old Trafford.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Nigeria, anakumbukwa kwa kufunga mabao 39 katika michezo 99 aliyocheza akiwa na klabu ya Watford, kati ya mwaka 2014 na 2017.
“Odion ni mchezaji mwenye uzoefu wa kutosha katika ligi ya England, natumai atasaidia mipango na matarajio tulionayo hadi mwishoni mwa msimu huu,” alisema meneja wa Man Utd Ole Gunnar Solskjaer.”
“Lengo letu ni kufanya vyema katika michezo iliyosalia hadi mwishoni mwa msimu huu, ninaamini nimetumia nafasi nzuri ya kufanya usajili kupitia dirisha dogo la usajili.”
Ighalo alihamia nchini China mwaka 2017, na awali aliitumikia klabu ya Changchun Yatai. Miaka miwiwli baadae alijiunga na Shanghai Shenhua, na alifanikiwa kufunga mabao 10 kwenye michezo 19.
Mbali na Ighalo, Man Utd pia imemsajili Bruno Fernandes kutoka Sporting Lisbon ya Ureno, katika kipindi cha dirisha dogo la usajili ambacho kilifungwa rasmi jana Januari 31.