Msemaji wa Klabu ya Simba, Haji Manara amesema kuwa anazo taarifa za uhakika kuwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera hajaondoka nchini badala yake anafanya kazi na AS Vita kinyume na kibali alichopewa na serikali.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akifanya mahojiano na vituo vya redio kadhaa, ambapo amesema kuwa Zahera aliaga kuwa anakwenda DR Congo lakini yupo hapa Dar es salaam anafanya kazi na AS Vita na hilo wanalijua.
”Niseme tu kwamba Zahera tunajua habari zake, hajasafiri na timu yake ya Yanga kwenda Iringa na wala hajaenda DR Congo kama alivyoaga, namwambia tu kuwa asisahau kibali chake cha kazi hapa ni kufanyakazi na Yanga sio AS Vita kwahiyo mamlaka zinajua na atajikuta matatani,” amesema Manara.
Akizungumzia mechi ya kesho dhidi ya AS Vita, Manara amesema kuwa Simba imejiandaa vizuri kuelekea mchezo wa klabu bingwa Afrika kesho Jumamosi saa 1:00 jioni kwenye uwanja wa taifa Dar es salaam.
Simba ipo nafasi ya mwisho kwenye Kundi D lakini ina nafasi ya kufuzu endapo itashinda mchezo wa kesho dhidi ya AS Vita huku Al Ahly na JS Saoura ambao watacheza Misri nao kutoa timu moja itakayofuzu endapo mmoja atashinda au kutoa sare.