Mkuu wa Idara Ya habari na Mawasilino ya Simba SC, Hajji Manara amewataka mashabiki na wanachama wa Young Africans kushtukia mpango wa viongozi wao, kwa kutaja majina ya viungo Claotus Chama kutoka Zambia na Gerson Fraga kutoka Brazil.

Viungo hao wamekua wakitajwa kuwa kwenye mipango ya kuhamia Young Africans katika kipindi hiki cha dirisha la usajili kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kama kulipa kisasi cha Bernard Morrison kutua Msimbazi.

Manara ametoa ufafanuzi kwa kusema mwaka jana 2019, Chama na wengine akiwamo Meddie Kagere waliongeza mkataba wa mwaka mmoja utakaomalizika Julai 2021.

“Mkataba wa awali wa Chama ulikuwa unaisha Julai 2020, mwaka jana aliongeza mwaka mmoja ambao sasa utamalizika 2021, pamoja na nyota wetu wengine wanaotajwa.”

“Yanga au timu yoyote kama wanamtaka Chama na wachezaji waliokuwa na mikataba walete barua ya kuomba kumsajili, sisi hatuweza kwenda kwa Feisal Toto mwenye mkataba na kumsajili,” amesema Manara.

Kwa upande wa Fraga, ambaye kwa sasa yupo kwao Brazil kwa mapumziko mafupi, amekanusha taarifa zilizozagaa kuwa ameuandikia barua uongozi wa Klabu ya Simba kuomba kuondoa kama ambavyo inadaiwa kupitia mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari.

Amesema bado yupo Simba na hajamaliza mkataba, na sasa yupo kwao kwa mapumziko mafupi na atarejea mapema kabla ya muda wa kuingia kambini.

“Hizo taarifa za kuandika barua si kweli, mimi ni mchezaji halali wa Simba, mkataba wangu umebaki miezi sita, nitarudi kuitumikia timu yangu kwa msimu ujao,” alisema kiungo huyo.

Kikosi cha Simba kitaingia kambini mwanzoni mw ajuma lijalo kuanza maandalizi mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi Namungo FC utakaopigwa Agosti 29 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, na kisha timu hiyo kuunganisha kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu uliopangwa kuanza Septemba 6, mwaka huu.

Kampuni ya Coca-Cola yaisaini dili Ufaransa, Uholanzi
Pro. Lipumba achukua fomu NEC