Mkuu wa idara ya habari na mawasilino ya Simba SC Haji Manara, ameandika ujumbe wa kuwafariji mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kufuatia kipigo cha bao moja kwa sifuri kilichowakutana jana Jumatatu, Oktoba 26.
Simba SC ilipoteza mchezo dhidi ya Ruvu Shooting jijini Dar es salaam, kwa kufungwa bao moja kwa sifuri, sawa na matokeo waliyoyapata kwenye mchezo uliotangulia dhidi ya Tanzania Prisons uliochezwa juma lililopita mjini Sumbawanga, Rukwa.
Manara ameandika ujumbe huo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii na kusema: Salaaam Wanasimba wenzangu!
“Kwanza nitoe pole sana kwa matokeo mabaya mfululizo tuliyoyapata kwenye michezo yetu miwili mfululizo.
“Haya sio mazoea yetu, sio Simba tunayoitaka sisi, lakini ndio ukatili wa huu mchezo ulivyo na kiukweli hatuna budi kukubali yaliyotokea!
“Ndugu zangu najua inauma sana, lakini Simba ni klabu yetu na hatuna klabu nyingine tuipendayo toka moyoni zaidi ya hii.
“Inaweza kufikirisha kidogo kama tunaweza kurudi katika nguvu yetu, lakini mimi Haji Manara nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kwamba msimu huu hatutachukua ubingwa.
“Muhimu ni kujikosoa pale ambapo labda tunadhani tunateleza na kutorudia makosa (Kama yapo), Ila mimi narejea kuwaambia inaweza kuwa upepo wa ukatili wa mchezo wenyewe wa mpira, ukizingatia katika mechi zote mbili tulipoteza nafasi kadhaa za kuweza kupata matokeo tofauti na tuliyoyapata!
“Kitu cha kufanya katika kipindi hiki kigumu kwetu ni kuwa na utulivu na kuwa wamoja, namaanisha UMOJA.
“Always (mara zote) Simba ikiwa MOJA huwa haishindwi hivi.
“Na kwa nini nasisitiza hili la UMOJA, hili tumeliandika katika mioyo yetu kama kauli mbiu yetu kuwa Simba Nguvu Moja, tukiliacha, hatujawahi kuwa Simba SC.
“Nimalizie kwa kuwaambia hiki ni kipindi mtacharurwa sana mitandaoni, maofisini na majumbani pamoja na vijiweni kwenu, ichukulieni hiyo ndio raha na karaha ya football, isiwasambue hata kama itawaumiza. Naamini soon (karibuni) itageuka kwao, hatujalala ndugu zangu na hatutalala!
“Mimi mitandao yote naona kama imenielemea binafsi lakini nipo strong (imara) na bado imani yangu kuhusu Marathon hii ndefu ni kwamba tunakwenda kuchukua ubingwa wa nne mfululizo. Inshaallah.”