Msemaji Mkuu wa Klabu ya Simba, Haji Manara amerusha dongo hewani kwa kusema kuwa kuna kikundi cha watu wachache ambao wanazijua Simba na Yanga katika mitandao ya kijamii na ndio maana wanaleta chuki za kijinga baina yao bila ya kujua wametoka wapi.
Ameyasema hayo kupitia ukurasa wake kijamii ikiwa imeambatana na ‘video’ iliyokuwa inamuonyesha mchezaji Haruna Ninyonzima (Simba), Thabani Kamusoko (Yanga) pamoja na Hamisi Tambwe (Yanga) wakiwa wanafanya mazoezi ya viungo katika ‘gym’ moja bila ya kujali tofauti ya itikadi zao za michezo.
“Very nice’, hawa ni ‘proffesional player’ hasa wanacheza timu shindani kwenye soka nchini, wanatoka mataifa tofauti lakini wapo ‘Gym’ pamoja hii ndio soka. ‘Always’ nawaambia Simba na Yanga ni washindani wa dakika 90 za uwanjani na watani wa jadi tu,” amesema Manara.
Amesema kuwa chuki zinazoletwa na baadhi ya watu ambao hawajui Simba na Yanga zimetoka wapi zinapaswa kupuuzwa.
Hata hivyo, Simba kwa sasa inaongoza katika msimamo wa ligi kuu Tanzania bara ikiwa na alama 46 sawa na watani wao wa Jadi Yanga zikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa pamoja na idadi ya michezo Yanga ikiwa mbele kwa mchezo mmoja.