Mkuu wa idaya ya habari na mawasiliano ya mabingwa wa soka Tanzania bara Simba SC Haji Sunday Manara, amewataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kupuuza taarifa zinazomuhusu kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chama.

Chama amekua akihusishwa na taarifa za kusukiwa mipango ya kuihama klabu hiyo ya Msimbazi na kusajiliwa na watani zao wa jadi Young Africans ambao wamedhamiria kukiboresha kikosi chao mwishoni mwa msimu huu.

Manara amesema kuwa Chama ni mali ya timu hiyo na hakuna mpango wa yeye kuibukia timu nyingine kwa sasa.

“Hizo ni habari tu ambazo zinaeleza kwamba Chama anaondoka anakwenda sijui wapi, lakini ukweli ni kwamba mwamba bado yupo ndani ya Simba na suala la kuondoka bado sana.

“Kwa sasa akili zetu tumeziwekeza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kisha mambo hayo mengine yatafuata,” amesema.

Simba inawakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa ambapo ina kazi ya kusaka ushindi mbele ya Plateu United ya Nigeria. Mchezo wa kwanza kwa Simba unatarajiwa kuwa nchini Nigeria Uwanja wa Jos kati ya Novemba 27-29 na ule wa marudio unatarajiwa kuchezwa kati ya Desemba 4-6, Uwanja wa Mkapa.

Cuhas kutafiti saratani kanda ya ziwa
Diwani afariki kabla ya kuapishwa