Mkuu wa idara ya habari na mawasilino ya klabu ya Simba Haji Sunday Manara, ametuma ujumbe kwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo, baada ya kupata matokeo mabaya ya kufungwa na Young Africans bao moja kwa sifuri jana Jumapili, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Haji ambaye kwa sasa yupo nchini Hispania, ametuma ujumbe huo kupitia ukurasa wake wa Instagram, kwa kuwataka mashabiki na wanachama wa klabu ya Simba kuwa watulivu, na kukubaliana na matokeo ya mchezo huo.
Haji amekiri Young Africans walicheza vizuri, na walistahili kushinda, hivyo ni jukumu la kila mwanachama na shabiki wa klabu ya Simba kujipanga upya kwa kuangalia michezo iliyosalia, kuelekea kwenye ubingwa wa msimu huu 2019/20.
Haji ameandika: Wanasimba wenzangu niwape salaam zangu fupi za kuwaomba kwanza tukubali tumepoteza mchezo wa jana kwa kufungwa na timu ilyocheza vizuri kuliko sie, na tukubali hilo halibadiliki kwa sasa,,najua tumeumia ila hyo ndio football tuliyoichagua kuipenda, kwa tamaduni zetu lazma tucharurwe kama ambavyo tungewacharura iwapo tungeshinda, but life goes on, Muhimu kujipanga kwa mchezo unaofuata keshokutwa, tusitoke ktk reli na sote tunajua ubingwa upo mikononi mwetu ,tusithubutu kumtafuta mchawi wala kulaumiana.
Wametufunga kihalali kabisa na ni haki yao kutamba!!
But Insha’Allah tutachukua ubingwa wetu. ???? #SimbaNguvuMoja
Hata hivyo baada ya ujumbe huo, mashabiki na wanachama wa klabu ya Simba SC walionyesha kukubaliana na Haji Manara, na kumuahidi wapo pamoja katika kipindi hiki ambacho wanaamini timu yao itaendelea kupambana ili kukamilisha lengo la kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo.
Simba bado wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Ya Soka Tanzania Bara kwa kufikisha alama 68, mchezo ujao watacheza dhidi ya Singida United Machi 11, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.