Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Sunday Manara, ameendelea kutaja thamani ya baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo, ambayo inatetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2020/21.

Mwishoni mwa juma lililopita Manara aliweka hadharani thamani ya kiungo kutoka nchini Zambia clatous Chama, baada ya mchezo huyo kuhusishwa na mipango ya kuhamia Young Africans mkataba wake utakapofikia kikomo mwishoni mwa msimu huu. Thamani ya Chama ilitajwa kufikia shilingi bilioni mbili.

Manara ameibuka upya na kuweka bayana thamani ya mshambuliaji  kutoka nchini Msumbiji Luis Miquissone, kwa kusema mchezaji huyo huenda akawa mchezaji ghali kwa sasa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Manara amesema waliangalia uwezo wa Miquissone katika michezo mbalimbali aliyocheza akiwa na kikosi cha Msumbiji, Orlando Pirates na UD Songo na kuvutiwa na kipaji chake.

“Tunajivunia kuwa na kikosi imara, kwa sasa Miquissone ndiye mchezaji ghali, na si kwa Simba tu, ni kwa Afrika Mashariki nzima, tumemnunua kwa dau nono, halijawahi kutokea, analipa kwa kile kiwango anachokionyesha,” amesema Manara.

Ameongeza klabu mojawapo ya Uholanzi ilionyesha nia ya kumnunua kwa dau la Euro 400,000, lakini Simba haikuwa tayari kumwachia kwa kiasi hicho cha fedha kilichotajwa.

“Kuna mawakala wa klabu moja ya Uholanzi walikuja kufanya mazungumzo na sisi (Simba), tena kwa hela nzuri ya Euro 400,000 ili kumnunua, lakini ‘Mo’, (Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohamed Dewji) akasema labda walipe Euro milioni moja (Sh. bilioni 2.6), kiasi walichotaka kwetu ingekuwa hasara,” Manara amesema.

Ameongeza kiungo huyo ni mali ya Simba na hajasajiliwa kwa mkopo kama baadhi ya klabu nyingine za hapa nchini zinavyoamini.

“Ni mchezaji wetu halali kwa asilimia 100, tena ana mkataba mrefu, hajaja kwa mkopo, tunamshukuru Senzo (Mazingiza- aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba), alisaidia sana kufanikisha ujio wake, hakuna ambaye anaweza kumpata,” Manara ameongeza.

Trump, Biden watupiana vijembe
Uwanja wa CCM Mkwakwani kujengwa upya