Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC Haji Manara amesema kamwe hawezi kuiomba radhi klabu ya Young Africans kwa kile kinachodaiwa kuichafua Brand ya klabu hiyo yenye maskani yake makuu katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es salaam.
Manara alipewa siku 14 na uongozi wa Young Africans kupitia kwa Makamu mwenyekiti wa klabu hiyo Fredrick Lugano Mwakalebela kuomba radhi kwa kuharibu Brand ya klabu hiyo tofauti na hapo atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.
Manara ametoa kauli ya kutokua tayari kuomba radhi mapema hii leo Alhamisi (Februari 25) alipokua akihojiwa kwenye kipindi cha michezo ya Sports Arena kinachorushwa na Wasafi FM.
Manara amesema hata angepewa siku milioni moja hawezi kuiomba radhi Young Africans kwa masuala yanayohusiana na utani, ambao umerithishwa kwa vizani na vizani vya klabu hizo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Siwezi kuomba radhi kwa masuala ya utani, kinachowasumbua Yanga kwa sasa ni ‘STRESS’ za Simba SC kufanya vizuri katika kila nyanja, wanaona ubingwa wa VPL wameshaupoteza, Simba imeingia hatua ya makundi Afrika, tumeifunga AS Vita kwao, tumeifunga Al Ahly hapa nyumbani, sasa kwa nini wasiwe na ‘STRESS’ za kumtaka Manara aombe radhi?” aliohiji Manara
Katika hatua nyingine, Manara amedai kuwa Young Africans wameanza, na yeye atamaliza kwani ana kesi sita juu ya viongozi wa klabu hiyo akiwemo Mwakalebela, Bumbuli na wengineo hivyo wakienda mahakamani ndio itakuwa vizuri kwani suala hilo lilishakabidhiwa kwa mwanasheria wa klabu ya Simba.
Amesema muda wowote kuanzia sasa Mwanasheria wa Simba SC anaweza kulitolea ufafanuzi suala la kesi inayowakabili viongozi wa Young Africans, hivyo wajiandae.
“Nimeshamwambia mwanasheria wa Simba SC kuandaa utaratibu wa kesi za kuishtaki Yanga, maana wao si wameanza, sisi tunamaliza. Pale kila mmoja ana kesi yake dhidi ya Simba SC lakini tuliamua kukaa kimya kwa sababu ya kuthamini uungwana.” Amesema Manara