Siku moja baada ya Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) kutoa taarifa za kuahirisha mchezo wa watani wa Jadi uliokua umepangwa kuchezwa Oktoba 18 mwaka huu, Mkuu Wa Idara Ya Habari Na Mawasilino ya Simba Haji Sunday Manara amezungumza kuhusu mabadiliko hayo.
TPLB walitoa sababu za kufanya mabadiliko ya tarehe ya mchezo huo na kuupeleka Novemba 07, kwa kuhofia baadhi ya wachezaji kukosekna kutokana na majukumu walionayo kwa sasa ya timu zao za taifa, hivyo huenda wataweza kuchelewa kutokana na baadhi yanchi kuendelea na zuio la kuingia na kutoka, kufuatia janga la Corona.
Manara amesema wamepokea taarifa hizo bila kipingamizi chochote na wanaheshimu maamuzi yaliyofanywa na Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) iliyo chini ya Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF).
Amesema kufuatia mabadiliko hayo kikosi chao ktaendelea na maandalizi kwa kucheza michezo miwiwli ya kirafiki, ili kujiweka sawa na michezo mingine ya Ligi Kuu kuelekea mpambano dhidi ya Young Africans Novemba 07.
“Timu inajiandaa na michezo mingine ya ligi hasa baada ya mchezo wetu wa dabi dhidi ya Young Africans kupelekwa mbele sisi hatuna cha kusema katika hilo kazi yetu ni kucheza.”
“Kwa namna ambavyo tumejipanga tutacheza michezo miwili ya kirafiki, ambapo moja utakuwa Oktoba 10, tutacheza dhidi ya Pan Africa halafu baadaye tutacheza mchezo mwingine Mlandegeya Zanzibar.”
“Tunaendelea kujipanga kwa ajili ya michezo mingine, na timu ipo tayari kwa ajili ya kupambana, masuala ya ratiba wenye mamlaka wanajua namna ya kupanga”. Amesema Manara.