Mabingwa wa soka nchini England Manchester City, wapo katika mazungumzo ya kutaka kumsajili kiungo wa klabu ya Società Sportiva Calcio Napoli (SSC Napoli) Jorge Luiz Frello Filho.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kituo cha televisheni cha Sky Italy, zimeeleza kuwa Manchester City, tayari wameshatuma ofa ya Pauni million 40 kwa ajili ya usajili wa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 26, lakini uongozi wa SSC Napoli umetaka kuongezwa kwa dau hilo, hadi kufikia Pauni milioni 44.
Manchester City walianza kumfuatilia kiungo huyo tangu msimu uliopita, na benchi la ufundi limempendekeza kuwa miongoni mwa wachezaji wanaopewa kipaumbele cha kusajiliwa katika kipindi hiki.
Jorginho, ambaye bado ana muda wa miaka miwili katika mkataba wake na klabu ya SSC Napoli, ameitumikia klabu hiyo ya mjini Naples katika michezo 36 ya msimu wa 2017/18, amefunga mabao matatu, likiwepo bao alilowafunga Manchester City wakati wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya mwezi Novemba mwaka jana.
Wakala wa kiungo huyo Joao Santos, amesema mchezaji wake anahitaji kuondoka nchini Italia na kwenda England kusaka changamito tofauti ya soka lake, hivyo anaamini mipango ya usajili wake itakamilishwa wakati wowote kuanzia sasa.
“Jorginho bado ana mkataba na klabu ya SSC Napoli, lakini kinachoendelea sasa ni mazungumzo ya uhamisho wake, ninaamini yatakamilika kwa mafanikio.
“Suala la kuvunjwa mkataba wake, sio tatizo kubwa, ninaamini Manchester City wana uwezo mkubwa wa kufanya hivyo, tusubiri na tuone mipango itakavyokua bada ya kukamilishwa kwa mazungumzo.
“Lakini, ninarudia kusema, itategemea na maamuzi ya uongozi wa SSC Napoli ambao bado una mkataba na Jorginho.
“Manchester City ni mabingwa wa soka wa England, na ni moja ya klabu zenye uwezo mkubwa kifedha barani Ulaya. Endapo SSC Napoli na Manchester City watafikia makubaliano ya kufanya biashara ya uhamisho wa mchezaji huu, tutazungumza mengi zaidi kuhusu hili.
“Kwa sasa sijasikia lolote linaloendelea katika mazungumzo ya pande hizo mbili, lakini ninatarajia siku kadhaa zijazo nitapata taarifa kutoka kwa viongozi wa SSC Napoli.” Amesema Joao Santos kuiambia televishesni ya Sky Italia.