Beki kutoka nchini Sweden, Victor Lindelof hatakua sehemu ya kikosi cha Manchester United kitakachoshuka dimbani leo usiku kwenye uwanja wa Old Trafford, kucheza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Young Boys ya Uholanzi.
Meneja wa Manchester United, Jose Mourinho amethibitisha taarifa za kutotarajia kumpanga beki huyo, kufuatia majeraha ya alioyapata akiwa kwenye mchezo wa ligi ya England mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Crystal Palace.
“Victor atafanyiwa vipimo kesho (Leo Jumanne), lakini kwa uezefu wa timu yetu ya madaktari wanahisi mchezaji huyo atakua na maumivu ya misuli ya paja, wakati tunasubiri majibu ya vipimo atakavyofanyiwa, nina uhakika atakua nje kwa kipindi kirefu.” Alisema Mourinho alipokua kwenye mkutano na waandishi wa habari.
“Siwezi kusema kama ataweza kuwahi kipindi cha michezo ya mwezi ujao wa Disemba, wasiwasi wangu tutamkosa kwa muda mrefu sana kutokana na majeraha yanayohisiwa kumsumbua, kama itatokea anawahi kupona na kurejea kikosini kwa kipindi hicho itakua furaha kwa kila mmoja, maana tutakabiliwa na michezo mingi.”
“Kwa hesabu za habaka haraka ninahisi huenda akawa tayari kucheza mwezi Januari, pindi tutakapokua tunakabiliana na Newcastle United, Januari 2.”
Kuumia kwa Lindelof, kunamfanya ajiunge na beki mwenzake kutoka nchini Argentina Marcos Rojo, ambaye kwa kipindi kirefu yupo nje ya uwanja.
Hali hiyo inaifanya Man utd kusaliwa na mabeki watatu pekee ambao watakua na jukumu la kucheza michezo yote iliyosalia hadi mwishoni mwa mwaka huu 2018.
“(Phil) Jones, (Chris) Smalling na (Eric) Bailly ndio mabeki waliosalia kwa sasa, sina budi kuwatumia kwa umakini mkubwa ili kuhofia balaa la majeruhi kuendelea kutuandama,” alisisitiza Mourinho.
Ushindi wa aina yoyote katika mchezo wa leo dhidi ya Young Boys utaiwezesha Man Utd kufuzu hatua ya 16 bora ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, huku wakiiombea mabaya Juventus ifungwe na Valencia.
Mabingwa wa soka nchini Italia Juventus wanaongoza msimamo wa kundi -H wakiwa na alama tisa, wakifuatiwa na Manchester United wenye alama saba, Valencia wanashika nafasi ya tatu kwa kumiliki alama tano na Young Boys wanaburuza mkia kwa kuwa na alama moja.