Kiungo kutoka nchini Brazil Casemiro ataukosa mchezo wa Ligi Kuu England wakati Manchester United itakapoivaa Sheffield United baadae leo Jumamosi (Oktoba 21) baada ya kushauriwa na klabu hiyo kubakia nchini kwao Brazil ili kuendelea kupata nafuu kutokana na tatizo la kifundo cha mguu.
Kiungo huyo wa kati alipata jeraha hilo wakati Brazil ilipotoka sare ya 1-1 na Venezuela lakini akatangazwa kuwa fiti vya kutosha kucheza dakika 90 katika kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Uruguay Jumanne iliyopita.
Casemiro alitarajiwa kurejea United juzi, lakini alishauriwa na klabu hiyo kusalia Brazil ili kumsaidia kupona.
Anatazamiwa kurejea Carrington mapema wiki ijayo, ingawa pia atakosa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya FC Copenhagen itakayofanyika Jumanne kwenye Uwanja wa Old Trafford kutokana na kufungiwa baada ya kadi nyekundu katika mechi waliyochapwa mabao 3-2 na Galatasaray.
United wameelezea jeraha la mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 kama suala dogo na kuna matumaini atakuwa fiti kwa ajili ya dabi ya Manchester itakayochezwa kwenye Uwanja wa Old Trafford Oktoba 29, mwaka huu.
Kocha, Erik ten Hag ana matumaini ya kumtumia beki wa kushoto, Sergio Reguilón kwa ajili ya safari ya kwenda Sheffield United baada ya raia huyo wa Hispania kukosa mechi nne zilizopita kutokana na tatizo la misuli ya paja.
Reguilon anayecheza kwa mkopo kutoka Tottenham Hotspur na alifanya mazoezi na kikosi huko Carrington Alhamisi pamoja na Sofyan Amrabat, ambaye alikosa mechi za Morocco dhidi ya Liberia na Ivory Coast wakati wa mapumziko ya kimataifa.
Raphaël Varane bado hana shaka baada ya kukosa ushindi wa United dhidi ya Brentford.
Majeruhi wa muda mrefu Lisandro Martínez, Luke Shaw na Tyrell Malacia bado hawajawa fiti huku Jadon Sancho akiendelea na programu ya mazoezi binafsi.