Endapo Klabu ya Atalanta ya Italia haitakubali kushusha bei ya Euro 70 kwa ajili ya mauzo ya Mshambuliaji wake, mabosi wa Manchester United wamepanga kuachana na mpango wa kutaka kumsajili Rasmus Hojlund katika dirisha hili la usajili linaloendelea barani Ulaya.
Taarifa kutoka tovuti ya ESPN zinaeleza kwamba Manchester United itatuma wawakilishi wake kwenda Italia kuangalia namna ya kuishawishi Atalanta ili ikubali kushusha bei kwa ajili ya mchezaji huyo na ikiwa itashindikana itaachana na mpango wa kumsajili katika dirisha hili.
Tayari kocha Erik Ten Hag ameshawasilisha jina la Mshambuliaji wa Eintracht Frankfurt, Randal Kolo Muani mwenye umri wa miaka 24, kama mbadala wa Hojlund.
Muani, alionyesha kiwango bora katika msimu uliopita ambapo alifunga mabao 23 kwenye mechi 46 za alizocheza akiwa Frankfut.
Hata hivyo, kwa Muani nako dau lake linaonekana kuwa kubwa zaidi ambapo Frankfurt inahitaji walau Pauni 80 milioni ili kumuuza staa huyo ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika ifikapo 2027.
Muani pia alionyesha moto wake katika mashindano ya Kombe la Dunia nchini Qatar mwishoni mwa mwaka jana, ambapo alikuwa miongoni mwa mastaa wa Ufaransa.