Klabu ya Manchester United imempa rasmi mkataba wa kudumu wa miaka mitatu, Gunnar Solskjaer baada ya kutumikia klabu hiyo kama kocha wa kipindi cha mpito tangu Desemba mwaka jana.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 46 alianza kukinoa kikosi cha Manchester United akichukua nafasi ya Jose Mourinho aliyetimuliwa baada ya timu hiyo kuzorota.

Solskjaer sio mgeni katika klabu hiyo, ameshaitumikia kwa misimu 11 kama mchezaji akifunga goli la ushindi mwaka 1999 katika fainali ya Ligi ya Mabingwa.

“Hii ni kazi ambayo siku zote nimekuwa nikiiota na nimefurahi sana kupata nafasi hii ya kuiongoza klabu kwa muda mrefu,” Solskjaer mewaambia waandishi wa habari.

“Tangu siku ya kwanza nilipofika hapa, nilijisikia niko nyumbani katika klabu hii maalum. Ilikuwa heshima kubwa kwangu kuwa mchezaji wa Manchester United na baadaye kuanza kazi yangu ya ukufunzi hapa,” aliongeza.

Alipopokea kijiti kutoka kwa Mourinho, klabu hiyo ilikuwa katika nafasi ya sita kwenye Ligi Kuu ikiwa nyuma kwa alama 11 dhidi ya waliokuwa kwenye nafasi nne za juu zaidi.

Lakini alifanikiwa kuipa ushindi mfululizo katika mechi zake sita kwenye Ligi na kuifikia rekodi iliyokuwa imeandikwa na Sir. Matt Busby.

Akizungumzia uamuzi wa klabu hiyo, Naibu Mwenyekiti Mtendaji, Ed Woodward alisema kuwa uteuzi wa Solskjaer umetokana na kubainika kuwa kweli anastahili.

“Tangu alipoanza kufanya kazi kama muangalizi wa timu Desemba mwaka jana, matokeo yake yanazungumza yenyewe,” BBC wanamkariri Woodward.

Lissu aielezea barua yake ya kudai mshahara wa kibunge
Rais wa Comoro achaguliwa tena kuiongoza nchi hiyo