Kiungo kutoka nchini Ghana Thomas Partey ameanza kuchukuwa nafasi katika vyombo vya habari Barani Ulaya, hukua kihusishwana mpango wa kutaka kutimkia Juventus, lakini mkongwe Paul Ince amewaambia Manchester United wafanye wanaloweza kunasa saini ya kiungo huyo wa Arsenal.
Partey mwenye umri wa miaka 30, ataruhusiwa kuondoka Emirates kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi kama itawekwa mezani ofa nzuri.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta anataka kufanya maboresho makubwa kwenye safu yake ya kiungo, ambapo kwa sasa amemruhusu Granit Xhaka kutimkia Bayer Leverkusen kwa ada ya Pauni 21.5 milioni.
Arsenal pia ipo kwenye nafasi nzuri ya kumtangaza Declan Rice kutoka West Ham kuwa ni kiungo wao mpya baada ya kukubali kulipa Pauni 105 milioni.
Kama Partey atabaki, basi atakuwa pacha wa Rice kwenye safu ya kiungo ya Arsenal kwa msimu ujao, lakini hilo litatokea kama hakutakuwa na ofa ya maana kwamba Arsenal inataka Pauni 30 milioni kwenye mauzo ya Partey, ambaye amebakiza mkataba wa miaka miwili kwenye kikosi hicho cha Emirates.
Klabu kadhaa za Saudi Arabia zinahitaji saini yake, lakini mwenyewe anavutiwa zaidi na uhamisho wa kwenda Juventus.
Arsenal itahitaji kutafuta mrithi wa Partey kama ataondoka na ndio maana wanafukuzia saini ya kiungo wa Southampton, Romeo Lavia, anayeuzwa Pauni 50 milioni.
“Nawatazama Casemiro, (Bruno) Fernandes, Christian Eriksen, ni wachezaji wazuri sana, lakini bado kuna kitu hapo na kama unahitaji kijana, basi bei yake ni kubwa,” amesema Ince.
“Sawa kuna mazungumzo mengi ya kuhusu Caicedo. Napendezwa na Franck Kessie wa Barcelona. Hapewi tu muda wa kucheza. Kuna hizi habari za Thomas Partey kuondoka Arsenal. Ukifikiria ile miezi sita ya kwanza kwenye msimu, Partey alikuwa moto uwanjani. Jorginho akaletwa kwa sababu, hapo akaanza kushindwa kupata nafasi. Na hapo ndipo ilipokuja shida kwa Arsenal ya kupata sare na kupoteza mechi. Ningependa mtu wa aina kama yake au Kessie.”