Meneja wa klabu ya Inter Milan, Roberto Mancini amelazimika kutoa ufafanuzi wa kina kufuatia maamuzi ya kumuuza kiungo kutoka nchini Croatia, Kovacic Mateo.

Kovacic, ambaye ni raia wa nchini Croatia, anatarajiwa kukamilisha usajili wa kujiunga na klabu ya Real Madrid hii leo kwa dau la Euro million 35.5.

Mancini, amesema ilimlazimu kutoa ruhusa ya kuuzwa kwa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21, kutokana na sheria za shirikisho la soka barani Ulaya UEFA kuibana klabu ya Inter Milan.

Amesema alikua hana njia mbadala ya kufanya zaidi ya kuafikia jambo hilo kufanyika klabuni hapo, kutokana na utaratibu wa Financial Fair Play (FFP) ambao umekua ukizibana klabu kutumia fedha za usajili kutokana na mazingira yaliopo.

Meneja huyo amelazimika kutoa ufafanuzi huo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wadau wa Inter Milan ambao alionyesha kukasirishwa na kitendo kilichofanyika mwishoni mwa juma lililopita cha kumuachia Kovacic.

Kwa nyakati tofauti wadau hao walinukuliwa na vyombo vya habari wakisema Mancini hakuitendea haki Inter Milan, kutokana na kukubali kufanya maamuzi ya kushtukiza tena katika nafasi muhimu ya kiungo.

Kovacic, anakua mchezaji wa pili anayecheza nafasi ya kiungo kuondoka klabuni hapo kwa mwaka huu, baada ya kuruhusiwa kwa kiungo kutoka nchini Uswiz mwezi januari, Xherdan Shaqiri aliyejiunga na FC Bayern Munich kabla ya kuelekea nchini England juma lililopita baada ya kusajiliwa na Stoke City.

Tetesi Za Usajili Wa Wachezaji Barani Ulaya
Diamond Azungumzia Barua Inayodai Tiffah Sio Mwanae