Roberto Mancini ametangazwa kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Saudi Arabia ikiwa ni majuma mawili baada ya kuachia ngazi kama Kocha Mkuu wa Italia.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 58 aliiongoza Italia kushinda taji la Euro 2020, wakiifunga England kwa Penati katika Fainali iliyofanyika kwenye Uwanja wa Wembley.
Mancini rasmi anaanza kazi hiyo akisaini mkataba hadi mwaka 2027.
Timu hiyo iliweka rekodi ya Dunia ya kutofungwa mechi 37, lakini pamoja na mafanikio hayo ilishindwa kufuzu kwa Kombe la Dunia 2022.
Mchezo wa kwanza tangu aanze kuifundisha timu hiyo utakuwa ni ule dhidi ya Costa Rica utakaofanyika Septemba 8 kwenye Uwanja wa St James’ Park, Newcastle.
Naamini hii ni nafasi kubwa kwangu, kupata uzoefu zaidi wa soka katika nchi mpya, hasa nchi hiyo kuwa na umaarufu mkubwa katika soka Asia,” alisema Mancini.
“Uwapo wa wachezaji maarufu duniani katika Ligi ya Kulipwa ya Saudia ni ishara kuwa ni hatua ya kukua kwa soka la nchi hiyo.”
Katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka jana ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Herve Renard, Saudi Arabia iliishtua dunia baada ya kuwachapa Argentina waliokuja kuwa mabingwa wa dunia kwa mabao 2-1 huko Qatar, lakini walishindwa kuvuka hatua ya makundi.
Mancini aliongoza Manchester City kutwaa taji lake la kwanza la Ligi Kuu ya England mwaka 2012 na pia aliwahi kuziongoza Fiorentina, Lazio, Inter Milan, Galatasaray na Zenit St Petersburg.