Bondia wa Ngumi za Kulipwa nchini Tanzania, mwenye mbwembwe na tambo nyingi, Karim Mandonga, amesema amefurahia matokeo ya pambano lake mwishoni mwa wiki hii dhidi ya Daniel Wanyonyi kutoka Kenya licha ya kwamba alichezea kichapo.
Akizungumza baada ya pambano hilo, Mandonga alisema haikuwa siku nzuri kwake na bahati ilimwangukia Wanyonyi lakini hakukosea kwa sababu hakupigwa kwa KO (Knockout).
“Siku ya leo [Jumamosi), naona ilikuwa bahati yake, lakini hakuna kitu ambacho nimekosea kama nimekosea angenipiga kwa KO(knockout), mimi nilimpiga yule kwa KO,” alisema.
Mandonga aliongeza kuwa hakuna alichokosea huku akisema kuwa mchezo ndivyo ulivyo ukimaliza kuna matokeo matatu ambayo ni suluhu, kushinda au kushindwa kwa hiyo amekubaliana na matokeo.
Katika pambano hilo la raundi 10 uzani wa Light Heavyweight, lililofanyika jijini Nairobi, Kenya Jumamosi usiku, majaji wote watatu walimpa Wanyonyi ushindi.
Jaji George Athumani alimpa Wanyonyi alama 100-80, Waycliffe Marende akampa 100-80 na Leonard Wanga 100-89.
Hilo lilikuwa ni pambano la pili kwa mabondia hao wa Afrika Mashariki kukutana, katika pambano la kwanza lililofanyika Januari huko huko Nairobi, Mandonga alimchapa Wanyonyi kwa TKO (Technical Knockout).
Wakati huo huo Mandonga anatarajia kupanda tena ulingoni Jumamosi (Julai 29) kuzichapa dhidi ya Moses Golola kwenye ‘Usiku wa Vitasa’ unaotarajiwa kufanyika jijini Mwanza.