Bingwa wa Mkanda wa WBC katika upande wa ngumi na mateke (Kick Boxing), Emmanuel Shija, ameiomba Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC), kuangalia upya sheria na kanuni ya mchezo huo.
Hatua hiyo imetokana na baadhi ya mabondia kwa sasa kuonekana wanacheza mapambano mara kwa mara bila kujali afya zao.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Shija amesema mabondia wanatakiwa kujali afya zao kwa kutopanda ulingoni mara kwa mara, kwa sababu ni hatari kwa afya zao katika siku za baadae.
Amesema baadhi ya mabondia wamekuwa wakicheza mapambano kila baada ya kipindi kifupi na kwa kufanya hivyo wanaweza kupata athari mbalimbali za kiafya baada ya kuacha mchezo huo.
“Niwaombe TPBRC kuangalia upya sheria au kutunga sheria nyingine itakayosaidia kupunguza athari hizo kwa mabondia hapo baadae kwa sababu ngumi ni mchezo wa hatari, sio wa vichekesho, pia ninaiomba serikali iendelee kuwekeza katika mchezo huu ili kuurejesha katika nafasi ya kwanza,” amesema Shija.