Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Karim Mandonga ‘Mtu Kazi’, amemwambia Promota wa pambano la Zanzibar, Tosh Sports Promotion kuwa atakwenda Zanzibar kwa lengo la kupigana kweli na mpinzani wake huku akisisitiza hana taarifa zozote za kufungiwa na Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC).

Mandonga ametoa kauli hiyo akiwa kwenye maandalizi ya pambano hilo linalotarajia kufanyika Agosti 27, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung, Zanzibar, huku kukiwa na taarifa za kuzuiwa kupigana kwa kipindi cha wiki sita kufuatia kupigwa TKO na Moses Golola wa Uganda.

Mandonga amesema kuwa hana taarifa zozote za yeye kufungiwa kutoka kwa kiongozi wa Kamisheni hiyo huku akisisitiza kuwa anaendelea na maandalizi yake ya pambano la Zanzibar ambalo amejipanga kwenda kupigana kweli.

“Unajua kwa sasa najiandaa na pambano langu la Zanzibar, nataka niende nikapigane kweli, namwambia Promota wangu Tosh Sports kuwa nimejipanga vizuri kuhakikisha nakwenda kutoa burudani kwa mashabiki wa mchezo wangu Zanzibar.

“Kuhusu hilo kufungiwa mimi sijui chochote kwa sababu sijapokea barua wala ya kiongozi wala simu kutoka TPBRC ikinielekeza kama nimefungiwa ndiyo maana nakwambia akili yangu ipo kwenye pambano langu la Zanzibar hivyo mpinzani wangu huyo Muller JR ajipange,” amesema Mandonga.

Gamondi: Tupo tayari kwa Ligi Kuu, CAF
Namungo FC mguu sawa Ligi Kuu 2023/24