Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema kuwa ukuaji wa uchumi unapaswa kwenda sambamba na kasi ya kukua kwa maendeleo nchini.
Ameyasema hayo wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza sabuni na vipodozi cha kampuni ya Keds Tanzania Limited ya nchini China, kinachotarajiwa kuanza ujenzi hivi karibuni.
Mwijage amesema hatua iliyofikiwa na kampuni hiyo ya ujenzi wa kiwanda hicho ni miongoni mwa kazi nzuri ya kujivunia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinnduzi (CCM), ya kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.
“Kiwanda hiki kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka huku mauzo ya kampuni yakiwa ni dola za Marekani milioni 33 kwa mwaka, hii inatoa matumaini ya kufikia lengo la Sekta ya Viwanda kutoa walau asilimia 40 ya ajira zote,”amesema Mwijage.
Aidha, amesema kwa Serikali itahakikisha  inaendelea na juhudi zake za kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini na kuhakikisha wanawekeza mikoa yote.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Cliord Tandari amesema kuwa uwekezaji huo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na Serikali kwa ujumla.