Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Kanda ya Dar es Salaam- Temeke imeiamuru kampuni ya Quality Group Limited kuwalipa waandishi wake wa habari wa zamani 23 iliowaachisha kazi mwaka 2017, jumla ya Shilingi Millioni 232,324,172.96.
Tume hiyo inayofanya kazi kama Mahakama ya Mwanzo ya Migogoro ya Kazi, imeiamuru kampuni hiyo inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu Yusufu Manji, kuwalipa waandishi hao kiasi hicho cha pesa, baada ya kuridhika kuwa ilivunja mikataba baina yao kwa kuwaachisha kazi bila sababu maalumu.
Tume hiyo imefikia uamuzi huo baada ya wanahabari hao kufungua shauri la mgogoro wa kikazi, wakipinga uamuzi wa kampuni hiyo kuwaachisha kazi kabla ya muda wa mikataba yao w miaka miwili waliyosainiana kuisha.
Wanahabari hao walikuwa wakifanya kazi katika gazeti la JamboLeo, lililokuwa likimilikiwa na kampuni ya Manji ya Quality Media Ltd, ambapo waliachishwa huku mlalamikiwa akitoa sababu kwamba alikuwa amesikia mambo mazuri kuwahusu wao.
Katika shauri hilo, wanahabari hao, Joseph Lugendo na wenzake 22 walidai kuwa waliajiriwa na mdaiwa huyo kwa nyakati tofauti kwa mikataba ya miaka miwili, lakini Septemba 19, 2017 hata kabla muda wa mikataba yao haujaisha, mdaiwa aliwaachisha kazi.
CMA imesema kuwa hapakuwa na sababu halali ya usitishaji wa mikataba ya walalamikaji kabla ya muda kuisha na kuwa sababu aliyoitoa mlalamikiwa ni kinyume cha kifungu cha 8(1) (d) cha Kanuni za Ajira na Mahusiano Kazini (Kanuni za Utendaji Bora) za mwaka 2007.
“Kwa hiyo katika kesi hii, kushindwa kwa mlalamikiwa kuzingatia masharti ya mkataba hususan kifungu cha muda wa usitishaji mkataba, anawajibika kumlipa kila mlalamikaji mishahara kwa miezi iliyokuwa imebakia ya mkataba wa ajira,” amesema msuluhishi.
“Mdaiwa anawajibika kuwalipa walalamikaji (wote kwa ujumla) jumla ya Sh232,324,172.96. Pia kila mlalamikaji sharti apewe hati cheti safi cha huduma. Walalamikaji walishindwa kuthibitisha madai mengine hivyo yanatupiliwa mbali.” ameongeza msuluhishi.