Bondia Manny Pacquiao, leo atazichapa na bingwa wa dunia wa WBA, Lucas Matthysse jijini Kuala Lumbar nchini Malaysia, pambano liitakaloshuhudiwa na maelfu ya wapenzi wa masumbwi.
Pacquiao ambaye ni Seneta nchini Ufilipino, leo anajaribu karata yake ya kwanza akiwa anapigana bila kuwa na kocha wake wa muda mrefu, Freddie Roach ambaye waliachana baada ya kupata matokeo tata ya kupigwa na bondia wa Australia, Jeff Horn.
Pambano kati ya Pacquiao na Matthysse linaweka historia ya kuwa pambano la pili kubwa zaidi la masumbwi kuwahi kufanyika nchini humo baada ya pambano kati ya Mohammad Ali na Joe Bugner mwaka 1975.
Wizara ya Mawasiliano na vyombo vya habari nchini humo imesema kuwa pambano hilo litaoneshwa moja kwa moja kupitia kituo cha runinga cha taifa na kutangazwa redioni.
“Baada ya miongo kadhaa, wapenzi wa masumbwi watapata nafasi ya kuangalia pambano la mabingwa. Pambano kubwa zaidi baada ya lile la Muhammad Ali na Joe Bugner,” imeeleza taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa mapema leo.
Matthysse ameahidi kupambana kufa na kupona kuhakikisha anaweka historia ya kumpiga Pacquiao ambaye anashikilia rekodi ya ubingwa mara nane wa uzito tofautitofauti akiwa ni yeye na Lennox Lewis pekee kwenye rekodi hiyo.
“Pacquiao anaaminika kuwapiga mabondia wa Mexico na kuitwa ‘The Mexicutioner’ lakini mimi sio wa Mexico,” alisema Matthysse ambaye ni raia wa Argentina.
Pacquiao anashikilia rekodi ya kushinda mara 59, kupoteza mapambano 7 na sare 2. Mapambano 39 alishinda kwa KO.