Bingwa wa masumbwi ya uzito wa Welterweight, Manny Pacquiao ambaye ni raia wa Ufilipino anayeshikilia mkanda wa WBA, usiku huu atatetea ubingwa wake dhidi ya bondia Mmarekani, Adrien Broner.
Pambano hilo litashuhudiwa leo alfajiri kwa majira ya Afrika Mashariki, litafanyika Las Vegas nchini Marekani katika ukumbi maarufu wa MGM Grand Garden.
Broner aka ‘The Problem’ mwenye umri wa miaka 29 ana rekodi ya kushinda mapambano 33 ambapo kati ya hayo alishinda 24 kwa KO, kushindwa matatu na kutoa sare moja (33-3-1, 24 KOs). Ameahidi kumtembezea kichapo Pacquiao ili ajipatie heshima ya kuwa nguli ndani ya siku moja.
Umri wa Manny Pacquiao ambao ni miaka 40 akiwa ameshapigana jumla ya mapambano 69 akipoteza saba na sare mbili (60-7-2, 39 KOs), unatajwa kuwa fursa ambayo Broner akiitumia anaweza kushinda pambano hilo.
Hata hivyo, Manny Pacquiao ameeleza kuwa amelichukulia pambano hilo kuwa ni pambano muhimu la kuidhihirishia dunia kuwa umri sio kikwazo kwake na amejipanga kushinda kwa KO.
“Umri sio jambo la kuzingatia kwangu. Bado nina nguvu na kasi ya masumbwi iko palepale. Nataka niudhihirishie ulimwengu kuwa umri sio kikwazo hata kidogo,” alisema Pacquiao ambaye ni Seneta nchini kwao.
Broner ni kiunzi kwa Pacquiao anayefukuzia kupata nafasi ya pambano la marudiano kati yake na Floyd Mayweather ambaye mwaka jana aliahidi kuwa atarejea na kuachana na kustaafu ili azichape na bondia huyo Mfilipino.
Wachambuzi wengi wa masumbwi wanampa nafasi Pacquiao kushinda pambano hilo. Hadi sasa kwa mujibu wa utabiri wa wachambuzi na mabondia mbalimbali, Broner anapewa 1/30 ya uwezekano wa kushinda.
Endapo Broner atashinda, itakuwa pambano lililoleta mshtuko wa hali ya juu (upset), itayompa biashara kubwa zaidi bondia huyo Mmarekani kwenye ulimwengu wa masumbwi.
“Ninyi mnampa nafasi zaidi Pacquiao, mara mnazungumzia pambano lake la marudiano na Mayweather, lakini hayo yote hayawezekani kwa sababu inabidi anipite mimi kwanza,” alisema Broner.
“Na usiku wa pambano nitawashangaza. Nimejiandaa kumpiga kwa KO mapema kabisa,” aliongeza.
Kwa upande wa Pacquiao, yeye alitumia vifungu vya Biblia akieleza kuwa hataki kujivunia nguvu au maarifa yake bali anamuachia Mungu, lakini anaamini atashinda kwa KO.