Mlinda Lango chaguo la kwanza la Mabingwa wa Soka Ujerumani FC Bayern Munich Manuel Neuer ameanza mazoezi na kikosi cha klabu hiyo baada ya kuwa majeruhi kwa muda wa miezi 10.

Neuer alivunjika sehemu ya chini ya mguu wake kutokana na ajali aliyoipata alipokuwa akicheza mchezo wa kuteleza kwenye barafu.

Mlinda Lango huyo mwenye umri wa miaka 37 ameanza mazoezi hayo pamoja na makipa wengine wawili wa Bayern wanaotumika kwa sasa, Sven Ulreich na Daniel Peretz.

“Imekuwa faraja kwa kweli kuona nimerejea tena uwanjani nikiwa na wachezaji wenzangu,” alisema Neuer aliyepata jeraha hilo Desemba, mwaka jana.

Neuer aliyeshinda mataji 11 ya Bundesliga na mawili ya Ubingwa wa Ulaya akiwa na Bayern, ameelezwa kuwa amechelewa kurejea dimbani kutokana na changamoto alizokutana nazo wakati wa kuuguza jeraha hilo.

Mkurugenzi wa Michezo wa Bayern, Christopher Freund alisema ni muda mfupi umesalia kabla ya kipa huyo kurejea kwenye kikosi cha kwanza ingawa hakutaja muda sahihi wa suala hilo.

Neuer ambaye ni mshindi wa Kombe la Dunia 2014 alikuwa nahodha wa Ujerumani mpaka alipopata majeraha hayo, alipokwenda kwenye michezo ya kuteleza katika barafu siku chache baada ya Ujerumani kushindwa kutinga hatua ya 16 bora kwenye Kombe la Dunia 2022 lililofanyika Qatar.

Simba SC na mbinu mpya kuibamiza Power Dynamos
Uongozi Tabora Utd wamshangaa Asante Kwasi