Wagonga nyundo wa jijini London West Ham United wamethibitisha kumsajili mshambuliaji wa pembeni kutoka nchini Ukraine Andriy Yarmolenko, akitokea Borussia Dortmund.
Dili la usajili wa mchezaji huyo limekamilishwa baada ya wakala wake Shbalii Vadim, kusafiri hadi nchini Uswiz ambapo kikosi cha West Ham Utd kimeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi, na kufanya mazungumzo ya mwisho na uongozi wa The Hammers.
Yarmolenko mwenye umri wa miaka 28, amejiunga na wagonga nyundo hao kwa kusaini mkataba wa miaka miaka minne, ambao utamuweka jijini London hadi mwaka 2022.
‘West Ham ni klabu kubwa na ina mashabiki wengi ulimwenguni kote, ninafarijika kuwa sehemu ya klabu hii ambayo inashiriki ligi pendwa duniani (Premier League),’ Amesema Yarmolenko alipohojiwa kwa mara ya kwanza na kituo cha televisheni cha klabu hiyo.
Kwa upande wa klabu ya Dortmund, nao wamethibitisha kuondoka kwa Yarmolenko kupitia kurasa za mitandao ya kijamii, huku wakimtakia kila la kheri mchezaji huyo katika maisha mapya ya soka lake.
Yarmolenko ameondoka Dortmund baada ya kuwepo klabuni hapo kwa msimu mmoja, akitokea Dynamo Kiev kwa ada ya Pauni milioni 23.
Yarmolenko anakua mchezaji watano kusajiliwa na West Ham Utd katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa ligi, huku West Ham Utd ikiwa chini ya meneja mpya Manuel Pellgerini aliedhamiria kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha klabu hiyo.
Wachezaji wengine ambao tayari wameshasajiliwa na West Ham Utd ni Ryan Fredericks, Issa Dip, Lukasz Fabianksi na Jack Wilshere.
Wakati huo huo ofa ya Pauni milioni 25 iliyotumwa na The Hammers kwa ajili ya usajili wa nahodha wa kikosi cha Newcastle Utd Jamaal Lascelles imekataliwa.
The Magpies wameikataa ofa hiyo huku wakiweka msimamo wa kutokua tayari kumuweka sokoni mchezaji huyo katika kipindi hiki, kutokana na kuhitajika kwenye mipango ya meneja wao Rafael Benitez.