Uongozi wa Simba SC umehamishia nguvu katika Usajili wa Mlinda Lango mpya wa kigeni atakayechukua nafasi ya Mlinda Lango mzawa Aishi Salum Manula ambaye atakuwa nje ya Dimba kwa zaidi ya miezi mitatu.
Manula anatarajiwa kuwa nje ya kikosi cha Simba SC, baada ya kufanyiwa upasuaji Afrika Kusini na huenda asionekane hadi mwezi Desemba mwaka huu, kwa mujibu wa taarifa ya madaktari wa klabu hiyo.
Hali hiyo ndio imewaongezea chachu Mabosi wa Simba SC kugeukia eneo la Mlinda Lango atakayekuwa namba moja akisaidiwa na Ally Salim kwani Benno Kakolanya tayari ameshapewa Thank You na huenda akaibukia Singida Fountain Gate.
Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’, amewataka mabosi wa Simba SC kufanya haraka usajili wa Mlinda Lango mpya kutokana na ripoti ya Manula sambamba na mabeki wawili wa kati, huku majina yanayotajwa ni Fabien Mutombora na Alfred Macumu Mudekereza wanaoidakia Vipers ya Uganda timu aliyowahi kufanya kazi.
Mbali na Walinda Lango hao, inaelezwa kuwa mabosi wa Simba SC wana jina lingine la Mlinda Lango kutoka Zambia ambaye hata hivyo hajatajwa wala kufahamika timu anayoichezea kwa sasa.
Simba SC pia inataka kusajili mabeki wawili watakaochukuwa nafasi ya Joash Onyango na Mohamed Outtara ambaye tayari ameshapewa “Thank You’ kama Sawadogo.
Simba SC Wanataka kurejea msimu ujao 2023/24 Uwanjani wakiwa na nguvu kubwa na si kinyonge kama walivyomaliza msimu wa 2022/23 na Hata usajili wao wanafanya kwa siri na tahadhari kubwa kuliko misimu yote iliyopita.
Kwa taarifa yako ni kwamba wameshakamilisha asilimia 80 ya mastaa wapya wanaowataka na sasa wanachomalizia ni malipo tu na kuweka sawa mikataba ndipo waanze kuachia makombora kuanzia juma lijalo.