Mlinda Lango la Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC Aishi Manula, amesema kitu anachofikiria kwa sasa ni kushinda tuzo ya kipa bora Afrika, kwa sababu kwa sasa yeye kuchukua tuzo ya kipa bora wa Tanzania ni kitu ambacho siyo cha kushangaza tena.
Manula ameyasema hayo baada ya kikosi cha Simba SC kukabidhiwa taji la Ubingwa jana Jumapili (Julai 18), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Manula amesema siku zote mchezaji mwenye malengo hujiwekea nafasi ya kushinda kitu kikubwa zaidi ya kilichozoeleka.
Amesema anaamini nafasi ya kuwa Mlinda Lango Bora Barani Afrika ipo, kutokana na klabu yake kupata wasaa mwingine wa kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika kwa mara ya nne mfululizo.
“Nimejiwekea malengo ya kuwa kipa bora wa Afrika, naamini hakuna kitakachonizuia kwa sababu nimejipanga kupambania hiyo nafasi.”
“Msimu wa 2020-21 nilijitahidi kupambana tuliposhiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, nilithubutu kuisogelea nafasi hiyo kwa kuwa miongoni mwa walinda lango waliofungwa mabao machache hatua ya makundi.”
“Msimu ujao nina nafasi nyingine ya kufanya makubwa zaidi ya ilivyokua msimu huu uliomalizika kwa timu yangu kufika hatua ya Robo Fainali.”
Kwa hapa nchini Manula ndio Mlinda Lango Bora kwa misimu miwili mfululizo, huku akiwa chaguo la kwanza kwenye kikosi cha timu ya taifa *Taifa Stars*.