Baada ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC kujihakikishia nafasi ya kucheza Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Mlinda mlango wa klabu hiyo Aishi Manula amesema wanatamani kusonga mbele zaidi kwenye michuano hiyo.

Manula ambaye mpaka sasa ameonyesha umahiri mkubwa wa kulinda lango la Simba SC kwenye michuano hiyo, amesema matamanio yao kwa sasa ni kucheza hatua za juu, zaidi ya Robo Fainali ambayo wanakwenda kucheza siku kadhaa zijazo.

Manula amesema: “Tumepambana na hatuwezi kujibweteka kuona tumemaliza kila kitu baada ya kufika hatua ya robo fainali, maana hiyo ni hatua ngumu, lazima tujipange kikamilifu ili tuzidi kwenda mbali zaidi ya hapa,”

“Ni kweli tumepambana kadri tulivyoweza hadi tulipofika, tukiungwa mkono na mashabiki ambao wamekuwa bega kwa bega na sisi kwa nyakati zote, bado tuendelee kuwaomba kwamba tuungane kwa umoja wetu ule ule ili kuona tunafika mbali zaidi ya robo fainali,”

“Ndio maana nasema bado tuna kazi ngumu hakuna kulala, tutapambana Caf, ligi kuu na ASFC ambazo vyote tulichukua taji msimu ulioisha na sasa tunahitaji kutetea kwa msimu huu,”

Wakati huo huo kikosi cha Simba SC kimeondoka nchini leo Jumanne (April 06) majira ya saa 9:25 alasiri kwenda nchini Misri kupitia Dubai.

Msafara wa kikosi hicho umeondoka na jumla ya wachezaji 25 ambapo utapumzika Dubai na kesho Jumatano (April 07) asubuhi utaondoka kwenda Cairo, Misri na kufika saa 4:05 asubuhi.

Simba inaenda Cairo Misri kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Hatua ya Makundi dhidi ya wenyeji wao klabu ya Al Ahly ya Misri mchezo ambao utachezwa Ijumaa ya (April 09).

Simba SC inaongoza msimamo wa ‘Kundi A’ ikiwa na alama 13, ikfuatiwa na Al Ahly yenye alama 08, huku AS Vita ikishika nafasi ya pili na Al Merrikh inaburuza mka kwa kuwa na alama 02.

Simba SC na Al Ahly zimeshafuzu hatua ya Robo fainali, hivyo mchezo wao wa Ijuma (April 09) utakua ni wa kukamilisha ratiba ya michezo ya ‘Kundi A’.

Dilunga afunguka alivyoitosa Young Africans
Niyonzima: Simba SC mjiandae kisaikolojia