Kamati ya pamoja, ya ununuzi wa pembejeo za zao la korosho na wazabuni wamesaini mkataba wenye thamani ya Shilingi 375.5 bilioni, kwa ajili ya ununuzi na usambaji wa pembejeo hizo kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2023/2024.
Zoezi hilo la utiaji saini, limefanyika mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas ambaye ameitaka kamati hiyo na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), kuhakikisha wanasimamia ipasavyo utekelezaji wa mikataba kama walivyokubaliana.
Kanali Abbas, amezitaka pande hizo mbili kuhakikisha kuwa hawawaonei huruma wazabuni hao na iwapo watashindwa kutekeleza mikataba hiyo kwa wakati, wachukuliwe hatua stahiki za kisheria.
“Serikali haitavumilia aina yoyote ya ucheleweshaji wa pembejeo, niwaombe Vyama Vikuu pamoja na Bodi ya Korosho kutekeleza majukumu yenu kwa uadilifu na weledi wa hali ya juu,” amesema Kanali Abbas.
Naye Katibu wa Kamati hiyo, Mohamedi Nassoro amesema mikataba hiyo ni ya kuagiza salfa ya unga tani 70,000 ya kukinga ubwiriunga, kiuatilifu kwa ajili ya ugonjwa wa Chule tani 200, na kiuatilifu cha Mbu wa Mikorosho na Minazi lita 600,000.
Viutilifu vingine ni, lita 100,000 kwa ajili ya ubwiriunga pekee, lita 200,000 kwa ajili ya vidung’ata, lita 1,800,000 kwa ajili ya kutibu blaiti na lita 500,0000 kutibu ubwirirunga.
Aidha, wazabuni hao wamepewa jukumu la kuagiza magunia million 6,700,000 na mabomba ya kupulizia elfu 6,500 na Serikali imeendelea kuweka jitihada kwenye kilimo cha korosho ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo ili ifikie tani 700,000 ifikapo mwaka wa fedha wa 2025/2026.