Taarifa za kuaminika ambazo Dar24Media #taarifabilamipaka tumezipata ni kuwa klabu ya Simba SC imemnasa beki Edward Charles Manyama na tayari amemwaga wino wa kandarasi ya miaka miwili.

Manyama ambaye alitamba na Namungo FC kabla ya kutua Ruvu Shooting katika dirisha dogo mwishoni mwa mwaka jana, inaaminika kuwa alikuwa katika mazungumzo  na mabosi wa Young Africans lakini wakati Wananchi wakihaha kumaliza naye ghafla Ma-mafia wa Simba SC wakaingilia dili hilo na kumsainisha mapema juma hili akiwa katika kambi ya Taifa Stars.

Kusainiwa kwa Manyama kunamaanisha vita ya nafasi sasa inakwenda kuibuka upand wa beki ya kushoto ya Simba SC, ambayo imeshikwa kwa muda mrefu na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ huku hatma ya beki mwingine Gadiel Michael ikiwa bado haijafahamika kama ataachwa ama kuongezewa mkataba klabuni hapo.

Hata hivyo mpaka sasa Uongozi wa Simba SC haujasema lolote kuhusu usajili wa beki huyo ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha Taifa Stars, kilichoshiriki Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ zilizofanyika mapema mwaka huu nchini Cameroon.

Manyama aliibukia Biashara United Mara inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, na safari yake ya kuelekea Namungo FC ilichagizwa na aliyekua Kocha wa klabu hiyo Hitimana Thiery, ambaye aliondolewa klabuni hapo mwishoni mwa mwaka 2020, kufuatia mambo kumuendea kombo.

Hitimana alitambua uwezo wa Manyama alipokua Mkuu wa Benchi la Ufundi la Biashara United Mara, kabla ya kutimuliwa na kuibukia Namungo FC mapema msimu uliopita.

Ruvu Shooting: Manyama hajasaini kokote
Hiki hapa kinachompeleka Mkude hospitali