Maofisa watatu wa Jumuiya ya Ulaya (EU) leo Februari 5, 2018 wamemtembelea Mbunge wa Singida Mashariki,(Chadema), Tundu Lissu anayeendelea na matibabu nchini Ubelgiji..
Katika taarifa aliyotoa leo, Lissu amewataja maofisa hao kuwa ni Mkuu wa Idara ya Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki katika Wizara ya Nje ya EU, Patrick Simonnet.
Wengine ni Mkuu wa Dawati la Tanzania EU, Marta Szilagyi, Vania Bonalbert ambaye ni ofisa wa ubalozi wa EU Tanzania anayeshughulikia masuala ya utawala bora na haki za binadamu na Hortensia May Lyatuu.
Amesema ujumbe wa maofisa hao mbali ya kumjulia hali walifanya mazungumzo ya masuala mbalimbali yanayohusu Tanzania.
Lissu alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 mnamo Septema 7, mwaka jana na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na siku hiyohiyo alihamishwa Hospitali ya Nairobi na kulazwa.
Januari 6, 2018 alihamishiwa Ubelgiji katika hospitali ya Chuo kikuu cha Leuven, anakoendelea na matibabu.