Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuchangamkia fursa zitokanazo na maonesho ya Viwanda ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ili kuwezesha ukuaji wa uchumi wa viwanda ambao Serikali inaujenga.

Ameyasema hayo mara baada ya kutembelea maonesho hayo yanayoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere, Viwanja vya Karimjee na Gymkana, ambapo amesema kuwa maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 39 wa Wakuu wa Nchi za SADC yamekamilika yakihusisha kuwepo kwa maonesho ambayo nchi wanachama wataonyesha Teknoloji, Ubunifu na bidhaa zao kutoka katika Viwanda vya nchi za SADC.

Amesema kuwa Serikali imetoa fursa kwa wafanyabiashara wakubwa, wa kati, wadogowadogo na wenye bidhaa zinazozalishwa kwa mikono kuja kuonyesha na kuchukua teknolojia kutoka nchi wageni ambao wapo nchini.

“Sisi kama Serikali tumetoa fursa kwa wale ambao wanafanya kazi na kuzalisha bidhaa zao kwa kutumia mikono kuja kuonyesha bidhaa zao ili ziweze kupata masoko kwa nchi wanachama wa SADC kwani nchi zote zinakuja hapa kuleta bidhaa mbalimbali kwa hiyo Watanzania wanatakiwa kutumia fursa hii kuwauzia wageni bidhaa zetu,”amesema Majaliwa.

Aidha, amesema kuwa maonyesho hayo ni muhimu kwani yamezikutanisha nchi za SADC kuja Tanzania kuonyesha bidhaa, teknolojia ya uzalishaji viwandani, pamoja na ubunifu katika kuzalisha bidhaa hizo, kwa Watanzania ambao hawajawahi kufika Namibia, Msumbiji, Malawi pamoja na nchi zingine za kusini mwa Afrika ni fursa kubwa kwao kuleta bidhaa zao ili ziweze kupata soko kutoka SADC.

“Maonyesho haya ya wiki ya Viwanda kutoka nchi wanachama wa SADC yana fursa nyingi kwa Watanzania kwani yatafungua milango mingi ya masoko kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, pia yatakuwa ya wazi kwa hiyo Watanzania wanatakiwa kutumia fursa hii kubwa kuona bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya hapa nchini na nchi wanachama kutoka Jumuiya hii,” amesisitiza Majaliwa

Hata hivyo, Waziri Mkuu, ameongeza kuwa Mkutano huo ni fursa kwa Watanzania kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuweza kukuza sekta hiyo na kuwawezesha wageni kutoka nchi wanachama wa SADC kuja kuwekeza.

“Watanzania tutumie pia fursa ya Mkutano huu wa SADC kutangaza vivutio vilivyopo nchini, ili tuweze kuleta watalii kuja kutalii hapa kwetu, banda la Wizara ya Maliasili na Utalii lipo, lakini kila Mtanzania popote alipo, kwa wakati wake, atumie muda wake kuwaeleza wageni ikiwezekana kuwapeleka kwenye maeneo ya utalii kwenda kutalii, aeleze kuhusu mbuga zetu kama vile Serengeti, Ngorongoro, Ruaha na Gombe, lakini pia Mlima Kilimanjaro, bonde la Olduvai Gorge na Fukwe zetu nzuri ili wageni waweze kutembelea maeneo haya,”ameongeza Majaliwa

Korea Kaskazini yaituhumu Marekani kwa uchochezi
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 7, 2019