Pongezi kubwa zimfikie Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kwa juhudi kubwa zinaoonekana za kuhakikisha jiji la Dar es salaam linakuwa safi katika nyanja zote, kimazingira, kitabia, kiafya na hata kimaendeleo, hizi zote ni juhudi na kujituma ambako kila mwenye nia nzuri na jiji la Dar es salaam atakupongeza kwa uthubutu wake.
Si rahisi kufikia na kutatua kero ya kila mmoja, lakini yeye umethubutu hata kuita makundi makundi ya wenye kero, pia mtu mmoja mmoja kwa lengo la kuwasikiliza na kutatua kero zao, tumeshuhudia akiwaita wagonjwa na kuwapatia tiba, walemavu, waliodhulumiwa haki zao na wengine wengi kwa lengo la kuhakikisha wanapata msaada na kuishi vyema katika jiji la Dar es salaam.
Leo ni tarehe 9 Aprili 2018 Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anakutana na akina mama waliotelekezwa na waume au wenzi wao na kuachiwa mzigo wa kulea watoto kufika ofisini kwake ili kutafuta suluhisho la tabia hiyo ya baadhi ya wanaume.
Tayari, mamia ya akina mama wa jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani wamekuwa wakimiminika katika ofisi za mkuu wa mkoa pamoja na watoto wao ili kueleza namna wazazi wenzao walivyowatelekeza.
Wakati haya yanajiri, ofisi za Dar24 Media zimekuwa zinapokea simu kadhaa pamoja na maandiko ya kumpongeza Mheshimiwa Makonda ambapo watu hao pia wamemtaka kuwa makini.
Wengi ya watoa tahadhari hao ni wanaume ambao wamejikita katika hoja ya kuwepo kwa tabia miongoni mwa akina mama ya kuwasingizia wanaume wasiohusika kuwa ndio waliowapa uja uzito.
“Akina mama wa karne hii hawaoni shida kumbambikizia mtoto mwanaume asiyehusika ilimradi alipata kuwa na uhusiano naye na kwa bahati anajimudu kimaisha,” amesema Jackson Mpondella wa Kimara.
Wakati huo huo, Hamisi Masudi wa Keko amesema “Mheshimiwa Mkuu wa mkoa anapaswa kujua kuwa wapo wanaume kadhaa ambao tunawajua wamesingiziwa watoto wasio wa kwao na wake zao wa ndoa kabisa. Tatizo hili ni kubwa zaidi ya linavyoonekana. Hakuna mwanaume ambaye anaweza kukataa damu take lazima iwepo sababu ya msingi kabisa.”
Pamoja na hayo mdau wetu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Baba Monica ametuandikia ujumbe ufuatao “najua kuna wamama wamejipanga kwenda kutushtaki kule kwa mkuu wa Mkoa wa Dar leo . Mkuu wa mkoa, pamoja na lengo lako zuri, napenda kuwapa tahadhari akina mama kuwa DNA itahusika sana.”
Ameendelea Baba Monica kwa kusema kuwa “shauri yenu kina mama pale itakapoonekana kuwa watoto mnaodai ni wetu ni wa rafiki zetu. Ni lazima mchukuliwe hatua za kisheria.
Hadi sasa tafiti za kisayansi zinaonyesha kuwa kati ya watoto sita wanaozaliwa, wanne sio wa akina baba wanaotajwa kuhusika.