Tanzania itakuwa mwenyeji wa Maonesho ya 21 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali yatakayofanyika kuanzia tarehe 2 hadi 12 Desemba, 2021 kwenye viwanja vya Rock City Mall, Jijini Mwanza.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika katika ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma.
Waziri Mhagama amesema kuwa, Maonesho hayo ya Nguvu Kazi au Jua Kali yamekuwa yakijulikana hivyo kwa sababu yanawalenga wajasiriamali wa kati na wadogo waliopo katika sekta isiyo rasmi na lengo kubwa la maonesho haya ni kuwawezesha wajasiriamali kurasimisha shughuli zao kwa kuwapatia fursa ya kutangaza bidhaa zao, kubadilishana taarifa, kukuza ujuzi, kukuza masoko ya bidhaa na kukuza teknolojia ya utengenezaji wa bidhaa pamoja na kuongeza fursa za ajira za staha nchini.
“Tanzania imekua mwenyeji wa maonesho haya mara tano na mwaka huu 2021 itakuwa ni mara ya sita ambapo maonesho hayo yatafanyika Mkoani Mwanza,” Amesema Waziri Mhagama
“Kwa kutambua umuhimu wa maonesho haya tunategemea kuwa na zaidi ya Wajasiriamali 1,000 kutoka Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda, Sudan ya Kusini na Tanzania ambao watashiriki katika maonesho haya ambapo Tanzania itawakilishwa na Wajasiriamali zaidi ya 450,”
Amesema kuwa, Serikali imeendelea kuhakikisha haiwaachi nyuma Wajasiriamali na imekuwa ikiwawezesha kushiriki katika Maonesho mbalimbali ya Kimataifa ikiwemo hayo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kwa jina la Jua Kali au Nguvukazi.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan imejipanga kufanikisha maonesho haya kwa lengo la kuwawezesha wajasiriamali wakiwemo vijana, wanawake na wenye ulemavu wanatumia fursa hii kutafuta masoko katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki,” Amesema Waziri Mhagama