Hatimaye mapacha wanaounda kundi la P Square, Peter na Paul wametangaza kuzika rasmi tofauti zao na kurejea kama zamani.
Taarifa za kuzika bifu hilo zimetolewa na Peter ambaye awali alionekana kama ndiye aliyechangia kwa kiasi kikubwa kusambaratika kwa kundi hilo akiingia katika ugomvi na ndugu zake Paul na Jude ambaye alikuwa meneja wao kwa muda mrefu.
Kupitia Instagram, Peter amepost kipande cha video akiwataka mashabiki kumlaumu yeye kwa yote yaliyotokea na kwamba wameamua kudumisha udugu wao na kurejea katika usimamizi wa kaka yao, Jude Okoye.
“Nataka kuwajibika kwa yote yaliyotokea na nawaomba radhi kwa dhati mashabiki wetu. Kwa kutuunga mkono muda wote katika safari hii, mnatudai mengi ziadi ya yale tuliyowapa na ninaomba radhi kwa hilo. Tumerudi sasa katika safari mpya na usimamizi mpya (Jude Okoye), muziki mpya na mawazo mapya,” inaeleza sehemu ya ujumbe mrefu aliouandika Peter kwenye Instagram.
Mapacha hao walikuwa katika ugomvi mkubwa kwa kipindi kirefu huku kila mmoja akitangaza kufanya kazi zake binafsi. Ugomzi wao ulikuwa gumzo katika tasnia ya muziki Afrika huku wasanii wakubwa kama 2 Baba Odibia wakieleza kuwa wamejaribu kuwapatanisha mara kadhaa lakini juhudi zao hazikuzaa matunda.