Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo ameiagiza Idara ya Uhamiaji kuongeza kasi, kulinda na kuwa na uadilifu katika ukusanyaji wa mapato yanayotokana na shughuli za kiuhamiaji ili kuweza kulisaidia Taifa katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli mbalimbali katika kituo cha Namanga, ikiwa ni pamoja na kukagua maeneo yanayotumika kwa uingiaji na utokaji wa wageni na wenyeji lengo ikiwa kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu wanaokamatwa mikoa mbalimbali nchini.

Aidha, Chilo pia amewataka askari hao kuongeza kasi ya misako na doria kwa usalama wa nchi yetu ili wananchi waweze kushiriki shughuli zao za kimaendeleo kwa amani na salama ikiwa ni adhma ya serikali kuona wananchi wanafanya shughuli zao kwa amani na usalama.

Akisoma taarifa mbele ya Naibu Waziri, Afisa Uhamiaji Mfawidhi wa Kituo cha Namanga, Mrakibu wa Uhamiaji, Prolimina Tairo amesema kuwa mapato yameshuka kutokana na janga la corona ambapo idadi ya wageni wanaoingia nchini imeshuka.

“Kuanzia mwezi Januari mpaka Mei Idara ya Uhamiaji katika Kituo cha Namanga tumekusanya jumla ya Dola za Kimarekani 180,780 tofauti mwaka jana kipindi kama hiki tulikua tumekusanya Dola za Kimarekani 450,000,” amesema Tairo.

Aidha jumla ya wahamiaji haramu 11 wamekamatwa katika Wilaya ya Longido wakati wa operesheni ya kukamata wahamiaji inayoendelea katika Mikoa yote iliyopo mpakani mwa Tanzania na nchi jirani.

Diamond: Ukimzingua Ali Kiba nitakuzingua, tuna chetu
Ally Hapi: Nipo tayari kwenda kokote