Mamlaka za usalama za Israel, imesema wameyashambulia maeneo ya kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza na miili ya wanamgambo 1,500 imepatikana katika miji ya kusini iliyokombolewa na jeshi, katika mapambano makali karibu na eneo hilo la Palestina.
Taarifa hiyo, inakuja wakati ambapo Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akitahadharisha kwamba kampeni ya kijeshi ya Israel kufuatia mashambulizi ya awali ni mwanzo wa vita virefu vya kuiangamiza Hamas na kuibadili Mashariki ya Kati kuwa eneo salama.
Aidha, idadi ya vifo nchini Israel imevuka hadi watu 900 kufuatia shambulizi baya kuwahi kutokea katika historia ya miaka 75 ya Taifa hilo, huku maafisa wa Gaza wakiripoti kuwa watu 687 wameuawa hadi kufikia sasa ambapo Jeshi la Israel limesema Wanajeshi wengine 123 wameuwawa katika shambulizi kubwa la Hamas.
Rais wa Marekani Joe Biden alitarajiwa kutoa kauli kuhusu hali nchini Israel hii leo Oktoba 10, 2023 huku Umoja wa Mataifa ukisema watu karibu 200,000 wameyakimbia makazi yao huko Gaza, tangu vita kuzuka na matarajio ya uhaba wa maji na ukosefu wa umeme ni jambo lisilokwepeka.