Afisa Habari wa Singida Big Stars, Hassan Massanza, amewatoa hofu Mashabiki wa Klabu hiyo kuhusu utambulisho wa wachezaji watakaosajiliwa ili kuongeza nguvu kwenye kikosi chao wakati wa Dirisha la Usajili.
Singida Big Stars inatajwa kufanya usajili wa wachezaji kadhaa tangu kufunguliwa kwa Dirisha Dogo la Usajili Desemba 16, lakini hadi sasa Uongozi wa Klabu hiyo haujathibitisha rasmi usajili wa wachezaji hao.
Massanza amesema ni kweli Klabu yao ipo kwenye hekaheka za usajili, lakini ni mapema mno kutaja majina ya wachezaji waliokamilisha usajili ama wanaoendelea na mazungumzo na Uongozi katika kipindi hiki.
Amesema kinachotakiwa ni Mashabiki kuendelea kuwa na Subra, kwani wachezaji watakaosajiliwa kipindi hiki wote watashiriki kwenye Michuano ya Kombe la Mapinduzi itakayoanza rasmi Januari 2023.
“Tumefanya usajili mzuri kulingana na mapendekezo ya benchi la ufundi na tunatarajia wachezaji hao kuonekana rasmi katika mashindano ya Mapinduzi kwa kupata nafasi ya kucheza,” amesema Massanza.
Wachezaji wanaotajwa kusajiliwa Singida Big Stars katika Dirisha hili la usajili ni Mshambuliaji wa Al Masry ya Misri, Francy Kazadi, ambaye ni raia wa DR Congo.
Wengine ni Ennock Atta Agyei, ambaye aliwahi kucheza soka nchini akitumikia kikosi cha matajiri wa Chamazi na Ibrahim Ajib kutoka Azam FC ambao wameachana naye rasmi.
Katika Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2023 Singida Big Stars ipo Kundi B, pamoja na timu ya Young Africans na KMKM ya visiwani Zanzibar huku wakitarajia kufungua pazia dhidi ya KMKM Januari 2, 2023.