Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Mpira wa Kikapu Mohamed Mbwana amesema uwepo wa wachezaji wa Kimataifa kwa ajili ya mashindano ya Kanda ya Tano Afrika utaongeza hamasa kwa vijana kupenda mchezo huo.
Kocha huyo aliita wachezaji 22 kwenye kikosi hicho na kuwajumuisha nyota wawili wanaocheza Taiwan na Marekani; Hasheem Thabeet na Atiki Ally kwa ajili ya mashindano hayo mwezi ujao.
Mbwana amesema kama nyota hao wawili wakipata nafasi ya kuja kushiriki michuano hiyo watachangia kwa kiasi kikubwa vijana kupenda mpira wa kikapu na kutamani mafanikio waliyonayo.
“Tumewaita wachezaji hao tukiamini wataongeza nguvu kwenye timu ya taifa, ukiwa na mchezaji kama Hasheem Thabeet ni faraja kubwa na ni heshima kwake yeye kuja kuitumikia nchi yake lakini pia ujio wake utakuwa na faida kwa sababu utaongeza hamasa,” amesema
Thabeet aliwahi kucheza ligi ya kikapu Marekani maarufu kama NBA na Ally anasoma Chuo cha Michezo Marekani ambapo anacheza kikapu.