Walalamikaji katika kesi ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, inayomkabili mfanyabiashara Marijan Msofe maarufu ‘ Papa Msofe’ na wenzake wanne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wamedaiwa kuonesha nia ya kutokuendelea namashtaka dhidi ya washtakiwa hao.
Hayo yamebainishwa na mmoja wa washtakiwa hao, Wenceslaus Mtui ambaye amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa akiwa gerezani amepokea barua kutoka kwa walalamikaji, iliyomuarifu kutokuwa na na nia ya kuendelea na mshtaka dhidi yao.
Mtui ambae amezungumza kwa niaba ya washtakiwa wengine na kudai amepokea barua hiyo Oktoba 1, mwaka huu na kuongeza kuwa nakala za barua hiyo zipo kwa Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP) na ofisi ya DCI, hivyo wameomba mahakama iwatajie tarehe za karibuni ili kufahamu suala hilo limeishia wapi.
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali, Faraji Nguka amedai mahakamani hapo kuwa hakuwa na taarifa kuhusu barua hiyo na haipo katika faili lake, hivyo ameshauri wawashitakiwa, kufuatilia suala hiyo katika ofisi ya DPP.
Hakimu Shahidi amesema barua hiyo imemfikia mezani kwake na alishauri ndugu wawashitakiwa, wafuatilie suala hilo katika ofisi za DPP.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi hadi Desemba 14 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.