Mwanasiasa Stanley Livondo wa Kenya, amedai kumekuwa na njama za kisiasa kummaliza Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kumaliza kipindi chake cha uongozi.

Akiongea wakati wa mkutano wa Mbunge Moses Kuria kukaribishwa nyumbani katika uwanja wa Thika, Livondo alisema mipango hiyo ilikuwa imepangwa mara mbili, mojawapo ya njama ilikuwa kudungua ndege ya Rais Uhuru wakati mmoja alipokuwa akitoka Kisumu huku mara ya pili ikiwa ni alipokuwa safarini kuenda Dubai na baadae marekani.

Livondo hata hivyo hakusema ni nani waliokuwa na njama ya kummaliza Rais lakini akadai njama hiyo ndiyo sababu ya tofauti kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.

“Unajua watu wanaulizana eti walikosana kwa nini . . . kama uko na ndugu yako na yeye anataka kukuweka chini akuangushe kwa ndege mara mbili utamsamehe? Rais alikuwa akitoka Kisumu ya kwanza, tena Rais alikuwa akielekea Marekani kupitia Dubai, ndege ikarudishwa chini kwa sababu walikuwa wanataka kuangusha chini,” alisema Livondo.

Livondo alisema watu wa Mt Kenya wanafaa kujihadhari sana kuhusu mwelekeo wanaochukua kisiasa kwani huenda ikawachukua miaka 50 tena kuwahi kuingia katika Ikulu iwapo hawatakuwa makini kuhusu wanayemuunga mkono.

“Watu wa Central ni wengi sana lakini wasipoungana watapigwa mshale wa kisiasa ambayo watapona baada ya miaka hamsini,” aliongea Livondo.

Moses Kuria pia aliwataka wakazi wa Mt Kenya kuweka masharti yao kwa wagombea wa urais mwezi Agosti. “Eti sisi tunaombwa kura ya Kiambu, Murang’a na Nyeri bure. Si tuwaambie kwanza wawekelee, hawa watapata kura na ushindi lakini sisi tutabaki na nini?” alisema Kuria.

Madai hayo mazito ya Livondo yamezua hisia mseto huku baadhi wakitaka akabiliwe ili kutoa taarifa zaidi na wengine hata hivyo wanasema matamshi kama hayo ni hatari wakati huu ambapo taifa linaelekea katika uchaguzi wa Agosti.

Ruto na Raila kufanya Serikali ya umoja baada ya Uchaguzi
Ado Shaibu:Tume huru ya Uchaguzi haikwepeki