Hatimaye marafiki wa marehemu Alex Murimi Nderi, maarufu DJ Lithium, wamethibitisha kwa kusisitiza kwamba marehemu rafiki yao hakusukumwa kujiua na mfanyakazi mwenzie yeyote bali alikuwa akisumbuliwa na msongo wa mawazo uliopelekea kuchukua hatua hiyo.
Wakizungumza na vyombo vya habari, marafiki hao wamejitokeza na kufichua kuwa marehemu Murimi alikuwa akipokea matibabu kwa takribani miaka miwili iliyopita ili kutibu changamoto hiyo ya kiafya.
Mmoja wa marafiki wa marehemu DJ Lithium, Amayayi Mutuku, ambaye alizungumza na The Standard alisema kwamba marehemu alikuwa wazi kuhusu mapambano yake dhidi ya msongo wa mawazo.
Aliongeza kuwa DJ huyo alifurahia kufanya kazi katika kituo cha Capital FM na hakuwa ameonyesha aina yoyote ya tofauti za kibinafsi na wafanyakazi wenzake, pia hakukuwa na shaka yeyote ya kwamba angeamua kujichukulia hatua hiyo kali dhidi ya uhai wake.
“Msongo wa mawazo humfanya mtu kujihisi yuko peke yake. Ilivunja moyo wangu kumuona katika hali hiyo, ingawa tulikuwepo maishani mwake na mara kadhaa alionekana kuwa sawa,” alisema mutuku.
DJ Lithium, alikutwa akiwa ameanguka akiwa katika maeneo ya kazini kwake ‘Capital FM’ Januari 19, 2022. Ambapo wafanya kazi wenzake walimchukua na kumkimbiza kwa haraka katika Hospitali ya Nairobi ambapo punde alipofikishwa hospitalini hapo alitangazwa kuwa amefariki.
Kwa mujibu wa wasimamizi wa kituo hicho, familia ya Lithium iliarifiwa kuhusu dharura hiyo na ilifika hospitalini muda mfupi baadaye.
Madaktari katika hospitali hiyo walijaribu wawezavyo kuokoa maisha yake lakini kwa bahati mbaya alifariki dunia.
“Alex alikuwa kiungo bora kwa timu kubwa ya Capital FM, alikuwa Dj na mtayarishaji, mcheshi na mwenye upendo mkubwa” alisema Danny Munyi, Mkurugenzi wa Vipindi wa Capital FM Kenya.
Inaelezwa kuwa marehemu aliacha ishara ambazo baadaye zilitoa taswira ya kuwa alidhamiria kujitoa mhanga kupitia kidokezo cha kwamba alikuwa akipambana na maisha ambayo kwa namna fulani aliyaelezea kwa kupitia jumbe ‘tweets’ zake za mwisho zinazoonyesha, alikuwa akipambana na msongo wa mawazo.