Baada ya virusi vya Corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu (covid -19) kuingia ukanda wa Afrika Mashariki mnamo mwezi Machi mwaka huu, marais wa nchi zinazounda ukanda huo wamekuwa wakichukua hatua tofauti za kukabili.
Wakati Rais wa Uganda, Rwanda na Kenya wakifunga baadhi ya shughuli kwenye nchi zao na baadhi ya miji kwa wiki kadhaa, Tanzania na na Burundi wameruhusu wananchi kuendelea na kazi kwa kuchukua tahadhari ikiwepo uvaaji wa barakoa.
Jana Mei 12 baadhi ya marais walikutana kupitia video kujadili njia za kukabiliana na janga la corona katika Ukanda huo huku kikihudhuriwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir.
Kwa upande wa Rais wa Tanzania, John Magufuli na Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza ambao wanaendelea na maandalizi ya uchaguzi mkuu mwaka huu, hawakuhudhuria kikao hicho huku wakiendeleza mapambano kwa kutoa elimu zaidi.
Katika kikoa hicho wamehimiza umuhimu wa kupeana taarifa, na wamependekeza kutumika mara moja kwa mfumo wa kidijitali wa ufuatiliaji na mfumo wa kuwafuatilia madereva wa malori.
Pamoja na kuzungumzia hilo pia wamezunguzia masuala mengine kadhaa yakiwemo ya kushuka kwa uchumi katika sekta muhimu kama kilimo, biashara, viwanda na utalii.