Mkutano wa marais wa nchi za kikanda umefanyika leo katika mji mkuu wa Angola, Luanda katika juhudi za kutafuta ufumbuzi wa ghasia za umwagaji damu eneo la mashariki mwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC.
Ofisi ya rais wa Angola, imesema rais Joao Lourenco amewaalika rais wa DRC, Felix Tshisekedi, Paul Kagame wa Rwanda, mpatanishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambaye ni rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta na mwenyekiti wa sasa wa jumuiya hiyo rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye.
Katika hatua hiyo, tangazo la ikulu ya Burundi limethibitisha leo kushiriki kwa Rais wake Ndayishimiye katika mazungumzo hayo yatakayosaidia kufanikisha mbinu za kutafuta amani ya eneo hilo inayosababisha hali ya sintofahamu kwa makundi ya kiraia yasiyo na hatia.
Msemaji wa Ikulu ya Kinshasa Patrick Muyaya alisema serikali ya nchi hiyo haitakubali kuzungumza na kundi la waasi la M23, hadi pale itakapokuwa imeondoka kikamilifu katika maeneo yote iliyoyakamata kwa mtutu wa bunduki.