Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ametaka kukutana na waandaji wa CRDB Marathon ili azungumze nao kufahamu majukumu yake kufuatia kupewa cheo cha ubalozi wa mbio hizo bila kufahamu kinahusiana na nini.
Kikwete ameyasema hayo hii leo Agosti 14, 2022 jijini Dar es Salaam, katika kilele cha mbio za Marathon katika Viwanja vya Farasi na kuamsha vicheko kwa wahudhuruaji wa mbio hizo wakiwemo washiriki kutoka Data Vision International, huku akimtaka Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, kuzungumza na umma uliopo mbele yake akidai una hamu ya kumsikiliza.
MARATHON: Waliochangia matibabu ya moyo wapewa neno
“Nimepewa cheo leo hata majukumu yake siyajui lakini maadam nimepewa ubalozi wa Marathon hao walionipa nitawaomba tukutane wanieleze maana yake nini na kinahusiana na nini, nikushukuru pia Makamu wa Rais kwa kuwa hapa uongozi ni kuwa karibu na watu umma huu una hamu ya kukusikiliza,” amesema Dkt. Kikwete.
Awali akizungumza na Dar 24, Afisa wa Miradi wa Data Vision International, Macmillan George amesema wameshiriki mbio hizo kama mojawapo ya juhudi za kuunga mkono makundi mbalimbali ya kijamii yenye mahitaji maalum kama sehemu ya utamaduni wao.
Amesema, “Tunaishukuru DataVision International kwa kutudhamini sisi DataVision Joggin Family na hii ni sehemu ya utamaduni wetu kuhakikisha tunashiriki masuala mbalimbali ya kijamii hasa yenye uhitaji.”
George ameongeza kuwa, mbali na uchangiaji huo pia marathon hiyo imewasaidia kujiweka sawa kiafya na kwamba tayari wamekubaliana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutumia Viwanja vyao kufanyia mazoezi yatakayowahusisha watu wa rika zote bila kujali jinsia.