Kocha mpya wa timu ya taifa ya Ivory Coast Marc Wilmots ameahidi kumshawishi aliyekua nahodha na kiungo wa timu hilo la Afrika magharibi Yaya Toure, ili atengue maamuzi ya kustaafu.

Yaya toure alitangaza kustaafu kuitumikia timu yake ya taifa mwaka mmoja uliopita, baada ya kuiongoza Ivory Coast katika vita ya kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka 2015.

Wilmots aliahidi kufanya kazi ya ushawishi dhidi ya Toure alipozungumza na waandishi wa habari katika mkutano maalum wa kutambulishwa kwake kama kocha mkuu, mjini Abidjan.

Alisema atahakikisha anatumia ujuzi wake wote wa ushawishi ili kufanikisha suala hilo, japo alikiri huenda likabeba changamoto kadhaa kutokana na maamuzi yaliyochukuliwa na mchezaji huyo.

Wilmots mwenye umri wa miaka 48, ametangazwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ivory Coast, baada ya kuachana na kikosi cha Ubelgiji mara baada ya fainali za Ulaya za mwaka 2016, ambapo kikosi chake kilitolewa kwenye hatua ya robo fainali kwa kufungwa na Wales.

Ivory Coast ilikua inanolewa na mfaransa Michel Dussuyer, ambaye aliamua kujiuzulu mara baada ya kushindwa kufikia malengo ya kuiwezesha nchi hiyo kutetea ubingwa wa Afrika, katika fainali za AFCON mapema mwaka huu.

Serikali kuboresha na kuimarisha ukuaji wa uchumi wa viwanda
Mwamuzi Adongo Aonywa